Powered By Blogger

Monday, August 22, 2016

TFF YAWASIMAMISHA WACHEZAJI WATANO 'VIMEO' LIGI KUU

Na John ndeki , DAR ES SALAAM

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limezitahadharisha klabu tano za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) juu ya kuwatumia wachezaji ambao imewasajili, lakini imebainika mbele ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji kwamba wanamatatizo kwenye usajili wao.
Klabu hizo ni pamoja na Majimaji ya Songea ambayo ina mchezaji anayefahamika kwa majina ya George Mpole ambaye pia amebainika kuwa ndiye Gerald Mpole wa Majimaji ya Songea amefungiwa kucheza soka kwa mwaka kwa kosa la kubadili jina akiwa na lengo la kufanya udanganyifu kwenye usajili. Majimaji imeagizwa kutomtumia mchezaji huyo kutoka Kimondo FC.
Mwadui FC ya Shinyanga; Mchezaji William Lucian aliyesajiliwa na Mwadui ya Shinyanga kutoka Ndanda ya Mtwara, naye amefungiwa mwaka mmoja kwa kosa la kusajili Mwadui FC ilihali akiwa hajamaliza mkataba na Ndanda. Mwadui isimtumie mchezaji huyo.
Mbeya City ya Mbeya; Mchezaji Saidi Mkopi, pia amefungiwa mwaka mmoja kwa kosa la kujisali timu mbili. Imebainika kuwa akiwa bado na mkataba na Tanzania Prisons ya Mbeya hivyo Mbeya City isi1mtumie mchezaji huyo.
African Lyon ya Dar es Salaam; Mchezaji Rehani Kibingu aliyesajiliwa na African Lyon ya Dar es Salaam, amesimamishwa kuchezea timu hiyo mpaka uongozi wa African Lyon kumalizana na Ashanti United ya Dar es Salaam kabla ya Agosti 27, 2016. African Lyon isimtumie mchezaji huyo kwa sasa.
Mbao FC ya Mwanza; Mchezaji Emmanuel Kichiba aliyesajiliwa Mbao FC, naye amesimamishwa mpaka Mbao watakapomalizana na Ashanti United ya Dar es Salaam, kabla ya Agosti 27, 2016. Mbao FC isimtumie mchezaji huyo kwa sasa.

FIFA YAWAPA KOZI YA UTIMAMU WA MWILI MAKOCHA WA TANZANIA


Na JOHN NDEKI, DAR ES SALAAM
SHIRIKISHO la Soka la Kimataifa (FIFA), kwa mara nyingine limeipa nafasi Tanzania kwa kutoa kozi maalumu ya utimamu wa mwili (Physical fitness) kwa makocha wa Tanzania wenye leseni kiwango B inayoanza leo Agosti 22, 2016. Kozi hiyo inayoendeshwa na mkufunzi kutoka FIFA, Dk. Praddit Dutta, raia wa India itafikia ukomo Ijumaa wiki hii.
Akifungua kozi hiyo, Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine aliishukuru FIFA kwa namna inavyoipa nafasi Tanzania katika kozi mbalimbali hususani za ukocha na uamuzi.
“Si kila nchi inapata privilege (fursa) kama hii. Bila shaka FIFA inatambua uwezo wa makocha wa Tanzania kwa sasa. Mjue kuwa FIFA ina watu wa kuwapa taarifa kila kona. Kama mngekuwa mnafanya vibaya, FIFA wangesema Tanzania bado, kwa hiyo kozi zisipelekwe… lakini inaonekana mnafanya vema, mngefanya vibaya msingefikiriwa,” alisema Mwesigwa aliyekuwa mgeni rasmi katika ufunguzi huo.
Mwesigwa amesema kwa kuwa FIFA ina malengo chanya na Tanzania kwa kutoa kozi mbalimbali ikiwamo hiyo ya physical fitness inayolenga kuwapa ujuzi makocha hao kuwajengea uwezo wachezaji kuwa na stamina.
Hivyo akawataka makocha wanaohudhuria kozi hiyo kutumia fursa hiyo ya mafunzo si kwa ajili yao peke yao bali kuendeleza ujuzi huo kwa wengine ambao hawakubahatika kuwa sehemu ya wateule wa FIFA.
Naye, Mkufunzi wa kozi hiyo, Dk. Dutta alisema: “Bila shaka Tanzania inakwenda kufungua ukurasa mwingine wa soka la weledi kwa kuwa na wataalamu mbalimbali katika ukocha na uamuzi. Mnachotakiwa ni kujitahidi kufanya vema na kozi nyingine nyingi zinakuja.”
FIFA kwa kushirikiana na Idara ya Ufundi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), chini ya Mkurugenzi Salum Madadi, imepitisha majina ya makocha 27 kuhudhuria kozi hiyo inayofanyika katika Hosteli ya TFF iliyoko kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Ilala jijini Dar es Salaam.

Makocha wanashiriki kozi hiyo ni Mohammed Muza, Samwel Moja, Nassa Mohammed, Jemedari Said, Oscar Mirambo, Wane Mkisi, Cletus Mutauyawa, Shaweji Nawanda, Kizito Mbano, Dennis Kitambi, Sebastian Nkoma, Fikiri Mahiza, Nyamtimba Muga, Nassor Mwinchui, Alfred Itaeli, Henry Ngondo, John Tamba, Kidao Wilfred, Luhaga Makunja, Mohammed Tajdin, Mohammed Silima, Salum Ali Haji, James Joseph, Kessy Mziray, Daudi Sichinga, Bakari Shime na Salum Mayanga.

WAZIRI NAPE AKABIDHIWA SHAMBA LA BIBI, LIGI KUU BYE- BYE TAIFA


Na john ndeki,DAR ES SALAAM
SERIKALI imekabidhiwa rasmi uwanja wa Taifa wa Uhuru, (pichani juu), jijini Dar es Salaam, leo Agosti 22, 2016, baada ya ukarabati mkubwa wa uwanja huo kukamilika.
Akipokea uwanja huo kwa niaba ya Serikali, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, amewapongeza wakandarasi ambao ni kampuni ya China ya Beijing Construction Engineering Group Company Limited, (BCEG), na mshauri mwelekezi wa uwanja huo kampuni ya kizalendo chini ya uongozi wa ke, Injinia Aloyce Peter Mushi kwa kazi nzuri iliyofanyika licha ya mikwamo ya hapa na pale.
“Ndugu zetu Wachina, wameonyesha sio tu uhusiano mzuri bali wameonyesha kuwa wao ni ndugu zetu, kwani walishiriki wakati nchi yetu ikipata uhuru laini toka wakati huo hadi hivi sasa, bado wanashiriki katika kusaidia kuimarisha uchumi wetu,” alisema.
Mwonekano wa Uwanja wa Uhuru baada ya ukarabati mkubwa .
Waziri Nanuye aliwataka watumiaji wa uwanja huo kulipa ada za matumizi kama inavyostahili, ili hatimaye fedha hizo ziweze kugharimia matunzo ya uwanja.
Akitoa taarifa ya ujezni huo, mshauri huyo mwelekezi wa ujenzi, Injinia Aloyce Peter Mushi alisema, uwanja huo una uwezo wa kuchukua watu milioni 22 na ulikamilika na kuanza kutumika kwa mara ya kwanza Mei 22, 2015.
Naye Meneja Mkuu wa Kampuni ya BCAG, Cheng Long Hai, alisema, uwanja huo umewekewa mifumo yote muhimu kama vile tangi la kuhifadhia maji na mifumo ya maji taka, na kuishukuru serikaliya Tanzania kwa kuiaminikampuni yake kutekeleza mradi huo mkubwa.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Elisante Ole Gabriel, alisema, amekuwa akipokea maombi mbalimbali ya wanamichezo na watu wengine kuomba kuutumia uwanja huo na kuwahakikishia kuwa utaratibu unapangwa ili watanzania waanze kufaidi matunda ya uwanja huo ambao kutokana na ukongwe wake ulipachikwa jina la shamba la bibi.
“Nitoe rai tu kwa watanzania, leohii Agosti 22, 2016 ambapo tumekabidhiwa uwanja huu rasmi ukiwa umekamilika, naomba hilo jina la shambala bibi nalo lifikie kikomo kwani uwanja huu sa sa unauonekano mpya na wa kisasa.” Alisema Profesa Gabriel.
Ukarabati huo mkubwa ulihusisha ujenzi wa jukwaa na paa, ikiwa ni pamoja na miundombinu mingine ya uwanja kama vile, mifumo ya kusambaza maji, na kutoa maji taka, uwekani wa tanki la kuhifadhia maji, pamoja na ujenzi wa vyoo vya kutosha uwanjani.
Baada ya Serikali kukabidhiwa Uwanja wa Uhuru sasa mechi zote za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kuanzia wikiendi hii zinahama Uwanja wa Taifa.

Sunday, August 21, 2016

OFFICIAL- JOEL CAMPBELL ATIMKIA NCHINI URENO



Sporting Lisbon ya Ureno imetangaza kumsajili kwa mkopo wa msmu mzima mshambuliaji wa Arsenal na Costa Rica Joel Campbell.
Campbell, ambaye ameifungia Arsenal magoli manne kwenye michezo 30 katika michuano yote kwenye msimu wa 2015-16, amejiunga na timu hiyo kwa mantiki ya kupata nafasi ya kucheza zaiidi katika kikosi cha kwanza.
Campbell ,24, alijiunga na Arsenal mwaka 2011 akitokea timu ya Deportivo Saprissa ya nchini Costa Rica na ameshatolewa kwa mkopo mara tano tangu ajiunge na Washika bunduki hao.
Msimu wa 2012-13, Campbell alipelekwa kwa mkopo kwenye klabu ya Ligue 1 ya Lorient, akafunga magoli manne kwenye michezo 27, kabla ya kupelekwa klabu ya Real Betis kwenye msimu uliopita..
2013-14 alienda Olympiacos, na kufunga mabao 11 ikiwemo kwenye mechi ya klabu bingwa dhidi ya Manchester United kwenye hatua ya 16 bora..
Alipelekwa tena kwa mkopo kwenda Villarreal msimu wa 2014-15, kabla ya kurudi tena Arsenal msimu uliopita.

UFAFANUZI KADI NYEKUNDU YA AJIBU MSIMU ULIOPITA, ILIMZUIA KUCHEZA DHIDI YA NDANDA?



````Baada ya mshambuliaji wa Simba Ibrahim Ajib kuitumikia klabu yake kwenye mchezo wa kwanza wa ligi msimu wa 2016/17 dhidi ya Ndanda FC, umezuka mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii kama nyota huyo alikuwa na uhalali wa kucheza game hiyo baada ya kupata kadi nyekundu mwishoni mwa msimu uliopita.
Ajib alioneshwa kadi nyekundu wakati Simba ikicheza dhidi ya Mwadui FC Jumamosi May 7, 2016 kwenye uwanja wa taifa mechi iliyomalizika kwa Simba kuchapwa na Mwadui bao 1-0. Ajibu alimkanyaga Hassan Kabunda wa Mwadui FC dakika chache kabla mechi hiyo haijamalizika na kujikuta akioneshwa kadi nyekundu na mwamuzi wa mchezo huo Anthony Kayombo.
Utata uliozuka ni kwamba, je Ajib alimaliza adhabu ya kutumikia kadi nyekundu aliyooneshwa na mwamuzi Anthony Kayombo?
Baada ya kadi hiyo, Ajib alikosa mechi tatu mfululizo za mwisho za ligi kuu Tanzania bara, mechi alizokosa ajibu ni Majimaji 0-0 Simba (11-05-2016), Mtibwa Sugar 0-1 Simba (15-05-2016) na mchezo wa mwisho wa ligi Simba 1-2 JKT Ruvu (21-05-2016).

Kwa mijibu wa kanuni za ligi, kanuni ambayo inahusu udhibiti na adhabu kwa wachezaji, kuna kipengele kinasema kwamba, mchezaji atakayetolewa kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja (straight red card) atakosa michezo miwili inayofuata.
Kifungu kingine cha kanuni hiyohiyo kinaongeza, mchezaji atakaeolewa kwa kadi nyekundu kwa kosa la kupiga au kupigana, atasimama kushiriki michezo mitatu inayofuata ya klabu yake na atalipa faini ya shilingi laki tano (500,000).
Kanuni hiyohiyo katika kipengele kingine kinasema kwamba, mchezaji atakaeoneshwa kadi nyekundu kwenye mchezo wa ligi kuu au atakaemaliza msimu wa ligi kuu akiwa na adhabu ambayo haijaisha muda wake, ataendelea kutumikia adhabu hiyo katika msimu unaofata isipokuwa adhabu inayotokana na kadi za njano.
Kulingana na takwimu hizo, Ajib alistahili kucheza mchezo wa ufunguzi wa ligi msimu wa 2016/17 dhidi ya Ndanda FC

SERENGETI BOYS YAFANYA KWELI, YAIPIGA AFRIKA KUSINI 2-0


Timu ya soka ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys imefanikiwa kusonga mbele katika Hatua ya Tatu kuwania kufuzu michuano ya Afrika kwa vijana ambayo itafanyika mwakani nchini Madagascar.


Serengeti ambayo katika mchezo wa kwanza wa Hatua ya Pili ya kuwania kufuzu michuano hiyo ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Afrika Kusini, leo imefanikiwa kusonga Hatua ya Tatu ya kuwania kufuzu michuano hiyo baada ya kuifunga Afrika Kusini mabao 2-0 katika mchezo wa marudio uliofanyika kwenye Uwanja wa Azam Complex nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.   

Kutokana na matokeo hayo Serengeti Boyimesonga mbele kwa jumla ya mabao 3-1.
 

RAIS MSTAAFU JK AONGOZA MAZIKO YA BI SHAKILA MBAGALA CHARAMBE JIJINI DAR.


Rais mstaafu wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ameongoza mamia ya wananchi kuuaga mwili wa mwanamuziki mkongwe wa taarabu Shakila Said Hamis maarufu kwa jina la ‘Bi Shakila’, leo jijini Dar.

  
Bi Shakila enzi za uhai wake.

Mwili wa Bi Shakila Said umehifadhiwa katika nyumba yake ya milele maeneo ya nyumbani kwake Mbagala Charambe jijini Dar.


Rais Mstaafu awamu ya nne, Dkt Jakaya Kikwete (wa tatu kulia) akijalidiliana jambo na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,  Nape Nnauye (pili kushoto).

Makamu wa Rais Mh, Samia Suluhu akijadiliana jambo na mmoja wa waombolezaji nyumbani kwa marehemu, kabla ya maziko kufanyika. Bi Shakila, amefariki ghafla nyumbani kwake, huko Mbagala Charambe.

 Rais Mstaafu Dkt Jakaya Kikwete akizungumza na waombolezaji.

Katibu MKuu wa Shirikisho la Wanamuziki Tanzania, John Kitime akiweka saini kitabu cha maombolezo cha Bi Shakila Said, nyumbani kwa marehemu Mbagala Charambe jijini Dar.

Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan akiweka saini kitabu cha maombolezo cha Bi Shakila Mbagala Charambe jijini Dar, kushoto ni  Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mh. Nape Nnauye.

 Baadhi ya wanamuziki wakongwe na Bongo Fleva wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kushiriki mazishi ya Bi Shakila huko nyumbani kwake Mbagala Charambe jijini Dar.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mh. Nape Nnauye akiwa na baadhi ya waombolezaji wengine wakiwemo wasanii wa muziki wa kizazi kipya, Banana Zorro na wanamuziki wakongwe wakiwa kwenye mazishi ya Bi Shakila, huko nyumbani kwake Mbagala Charambe jijini Dar.

APUMZIKE KWA AMANI, AMINA!

PICHA: MICHUZI-MATUKIO

BRAZIL WANYAKUA MEDALI YA DHAHABU OLIMPIKI SOKA, WAINYOA UJERUMANI KWA MATUTA


  • Wachezaji wa Brazil wakiongozwa na Nahodha wao, Neymar (katikati) wakishangilia baada ya kushinda Medali za Dhahabu za Michezo ya Oilimpiki 2016 Uwanja wa Maracana mjini Rio usiku wa jana kufuatia ushindi wa penalti 5-4 baada ya sare ya 1-1. Brazil ilitangulia kwa bao na Neymar dakika ya 27, kabla ya Max Meyer kuisawazishia Ujerumani dakika ya 59. Neymar akaenda kupiga na kufunga penalti ya ushindi, baada ya mkwaju wa Nils Petersen kuokolewa
  • AGUERO NA NOLITO WAPIGA MBILI-MBILI CITY IKIITWANGA STOCK CITY BRITANIA



    Manchester City chini ya Guardiola wakiwa ugenini wameendeleza wimbi lao la ushindi baada ya kuifumua Stock City mabao 4-1.
    Sergio Aguero na Nolito kila mmoja amefunga magoli mawili na kuipa City ushindi huo mnono na kuendelea kupambana kileleni na mahasimu wao Manchester United.
    Goli la Stock City lilifungwa na Bojan Krkic.
    Kauli za makocha baada ya mchezo
    Bosi wa Stoke City Mark Hughes amesema: “Penati zilikuwa muhimu, hasa ile moja ambayo ilikuwa dhidi yetu kwenye kipindi cha kwanza. Kuna mabadiliko makubwa sana ya sheria kwenye msimu huu wa ligi. Ilitutoa mchezoni kabisa.
    “Penati yetu pengine kama ingekuwa msimu uliopita isingetolewa, lakini ilitusaidia kurudi mchezoni mpaka tulipofungwa goli la tatu na kutoka kabisa mchezoni kabisa. Lakini siamini kama matokeo haya yameakisi mchezo ulivyokuwa.
    “Kiukweli kwa mwaka huu Man City ni klabu kubwa hasa, na hatukuweza kupambana nao kutokana na kasi waliyokuwa nayo.”
    Meneja wa Manchester City Pep Guardiola amesema: “Nafahamu vizuri namna gani wachezaji walivyo na ubora, najisikia ni mwenye bahati kubwa kutokana na ubora wa wachezaji niliokuwa nao hapa.
    “Wanacheza mpira kwa kasi, wanakaba, na leo tumecheza katika moja ya viwanja vigumu sana kwenye ligi hii. Imenisikitisha kidogo kwamba tumetengeneza nafasi nyingi kipindi cha pili lakini hatukuweza kumalizia vizuri.

    SIMBA YAANZA NA MOTO LIGI KUU, YAICHAPA 3-1 NDANDA…TSHABALALA APIGA SOKA YA NGUVU

    Na john ndeki, DAR ES SALAAM
    SIMBA SC imeanza Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa kishindo kufuatia ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Ndanda FC ya Mtwara jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Japokuwa hakufunga hata bao moja, lakini beki wa kulia Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ndiye anastahili sifa zaidi kwa ushindi mnono wa Simba leo, kutokana na kuseti mabao yote. 
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Emmanuel Mwandembwa wa Arusha, hadi mapumziko timu hizo zilikuwa zimefungana bao 1-1.
    Simba SC walitangulia kwa bao la mshambuliaji kutoka Burundi, Laaudit Mavugo dakika ya 20 aliyemalizia mpira wa adhabu wa Tshabalala.
    `Mshambuliaji anayeinukia vizuri nchini, Omary Mponda akaisawazishia Ndanda FC dakika ya 37 kwa kichwa akimalizia krosi ya Nahodha Kiggi Makassy.
    Mabadiliko yaliyofanywa na kocha Mcameroon wa Simba, Joseph Marius Omog kipindi cha pili akiwatoa Jamal Mnyate na Ibrahim Hajib na kuwaingiza Mwinyi Kazimoto na Frederick Blagnon  yaliiongezea uhai Simba na kuvuna mabao zaidi.
    Mshambuliaji kutoka Ivory Coast, Blagnon alianza kuifungia Simba SC bao la pili dakika ya 73 kwa kichwa akimalizia kona ya Tshabalala.

    `
    Nyota wa mchezo wa leo, Tshabalala akaseti bao la tatu baada ya kupiga kona iliyotemwa na kipa Jackson Chove na winga Shizza Ramadhani Kichuya akasukumia nyavuni kuipa Simba SC ushindi wa 3-1.

    Kwa ujumla Simba SC imecheza leo na ilistahili ushindi huo, wakati Ndanda walionyesha upinzani kwa wenyeji kipindi cha kwanza pekee. 
    Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Vincent Angban, Hamad Juma, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Novaty Lufunga, Method Mwanjali, Jonas Mkude, Shizza Kichuya/Mohamed Ibrahim dk84, Muzamil Yassin, Laudit Mavugo, Ibrahim Hajib/Frederick Blagnon dk62 na Jamal Mnyate/Mwinyi Kazimoto dk69. 
    Ndanda FC; Jackson Chove, Azizi Sibo/Bakari Mtama dk65, Paul Ngalema, Kiggi Makasi, Hemed Khoja, Salvatory Ntebe, Forahim Isihaka, Bryson Raphael, Salum Telela, Omary Mponda na Shija Mkina/Nassor kapama dk65.

    BOCCO AINUSURU AZAM FC KULALA KWA AFRICAN LYON CHAMAZI, SARE 1-1


    Na JOHN NDEKIN, DAR ES SALAAM
    BAO la Nahodha John Raphael Bocco dakika ya 93 usiku huu limeinusuru Azam FC kulala mbele ya African Lyon baada ya kupata sare ya 1-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
    Bocco alifunga bao hilo lililokuwa likisubiriwa kwa hamu akimalizia pasi nzuri ya kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’.
    Lyon walitangulia kwa bao lililofungwa na Mganda Hood Abdul Mayanja dakika ya 46 baada ya kuchonga kona iliyoingia moja kwa moja nyavuni.


    Sifa zimuendee kipa wa Lyon, Youthe Rostand aliyeokoa michomo mingi leo na ya hatari kabla ya kukubali bao la dakika ya 93.
    Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Aishi Manula, Ismail Gambo/Mudathir Yahya dk46, Bruce Kangwa, Himid Mao, David Mwantika, Jean Mugiraneza, Salum Abubakar ‘Sure Boy’/Francesco Zekumbariwa dk64, Shomary Kapombe, Frank Domayo/Kipre Balou dk63, John Bocco na Shaaban Idd.
    Afrcan Lyon; Youthe Rostand, Baraka Jaffar, Khalfan Twenye, Hamad Waziri, William Otone, Omar Salum, Hamad Manzi, Mussa Nampaka, Omar Abdallah/Abdul Hilal dk86, Hood Mayanja na Tito Okello. 

    HATIMAYE BENTEKE ATUA CRYSTAL PALACE.


    Klabu ya Crystal Palace imethibitisha kumsajili mshambuliaji Christian Benteke kutoka Liverpool kwa ada ya pauni milioni 32 ambayo ni kubwa kuwahi kutokea kwa klabu hiyo kusajili.
       



    Benteke alikuwa jijini London tangu jana Ijumaa kwa ajili ya vipimo vya afya ambapo baada ya kukamilisha taratibu alitambulishwa rassmi.


    Usajili huo umekuja baada ya mchezaji huyo kutokuwa katika wakati mzuri kwa kushindwa kutamba Liverpool tangu alipotua akitokea Aston Villa.

    Akizungumzia juu ya usajii huo, Benteke ambaye ana umri wa miaka 25 alisema: “Nina furaha kutua hapa Crystal Palace, nategemea kufanya mengi kwa kujituma.”

    Benteke amefunga mabao mabao 51 katika Premier League katika misimu minne aliyocheza katika ligi hiyo.

    MESSI SIYO SOKA PEKE YAKE, NI RIZIKI YA WATU WA JIJI LA BARCELONA



    LIGI Kuu Hispania maarufu kama La Liga imeanza kutimua vumbi huku kukiwa na mengi ya kuwaza au kubashiri, lakini hauwezi ukaizungumzia bila ya kumtaja Lionel Jorge Messi raia wa Argentina.

    Messi ndiye kipenzi cha watu wa Barcelona, mji wenye wakazi wapatao milioni mbili kwa sasa ambao pamoja na kuwa na kila aina ya biashara, wanaamini maisha yao kwa kiasi kikubwa yanaendeshwa na kikosi cha Barcelona na tegemeo lao kubwa kwa miaka mingi sasa, wanamtegemea zaidi Messi.

    Baadhi ya wafanyabiashara ambao wamefanya kazi hiyo kwa zaidi ya miaka kumi katika Jiji la Barcelona, wanasema hata wakati Luis Figo anatamba au Ronaldinho, hawakuwahi kuwa na biashara nzuri kama kipindi hiki cha Muargentina huyo ambaye heshima yake ni kubwa kuliko mtu yeyote anayeishi katika mji huu.

    Inajulikana, adui namba moja wa Mji wa Barcelona ni Cristiano Ronaldo wa Real Madrid na shujaa ni Messi. Kwani kila anapofanya vizuri uwanjani, anaisaidia klabu yake ya Barcelona kuingiza mamilioni ya fedha kupitia wageni wanaotembelea Camp Nou, wananunua bidhaa na kadhalika, yote ni fedha.

    WATEJA WAKICHAGUA JEZI ZA MESSI KWENYE DUKA LA BARCELONA. PICHA NA SALEH ALLY

    Kufanya kazi vizuri kwa Messi, kunaposaidia kuongeza wageni ndiyo faida kubwa kwa wafanyabishara wa jiji hili la Barcelona ambalo ni kati ya miji inayovutia sana barani Ulaya kutokana na kuwa na mpangilio mzuri sana na mvuto wa juu kabisa.

    Wanaouza jezi au fulana za Messi baada ya kuzinunua kihalali kwenye Klabu ya Barcelona, wamekuwa wakipata faida kubwa ingawa inaelezwa kuna katazo kutoka Kampuni ya Adidas inayomdhamini Messi. Haitaki kutoa fulana nyingi kwa kuwa inaona zitachangia kuchuja kwake.

    Watu wanashindwa kufyatua kwa kuwa ukikamatwa huku hakuna mchezo, ni jela au faini inayoweza kukulazimisha kuuza magari yako au kukumaliza kabisa kibiashara.

    Wafanyabiashara wa jezi za Messi ambazo ni halali nao wanapata biashara na zimekuwa ni ‘hot cake’ kwao au biashara inayotoka sana kuliko nyingine yoyote.

    Awali Barcelona ilitenga hadi euro 650,000 (zaidi ya Sh bilioni 1.5) kwa ajili ya promosheni ya biadhaa zake, lakini iliamua kuzitoa jezi au vifaa vya Messi kwa kuwa vimekuwa vikijitangaza, kujiuza na hata kuvitangaza vingine.

    Dereva taksi wa eneo la Sans katika jiji hili, Alejandro Garcia anasema wateja wake wengi wamekuwa wakimzungumzia Messi kila wanapoingia katika taksi yake.


    Amesema anapenda mpira, lakini katika miaka yake yote 44 sasa ya kuishi Barcelona, hajawahi kumuona Messi ambaye alifika jijini hapo akiwa na miaka 13.

    “Amenikuta hapa, lakini sijawahi kumuona. Ni vigumu sana kumuona lakini kila mtu anamuulizia. Anasaidia sana biashara yetu, tunaamini watu wengi hufurahia kufika hapa wakiamini ni sehemu anayoishi Messi,” anasema.

    Messi ni mfalme wa Barcelona, hakuna anayeweza kukataa. Ukiachana na wauza jezi, hata wenye mahoteli, wanasema watu wengi hufika katika Mji wa Barcelona ili kuutembelea Uwanja wa Camp Nou lakini gumzo kubwa limekuwa ni Messi.

    Inaonekana pamoja na uwezo wa soka, Messi amegeuka kuwa msaada kibiashara katika maisha ya wakazi wengi wa Barcelona kutokana na kuwa na tabia ya aina yake kabisa.

    Anapenda kujificha, hapendi makuu, zaidi ya mpenzi wake, Antonio Rucuzzo waliokua pamoja katika Mji wa Rosario kwao, Argentina, hajawahi kusikika hata kubadilisha tu mpenzi.

    Hii kwa wazazi wengi wa Ulaya hupenda kuona watoto wao wanakuwa kama Messi. Hivyo kufanya idadi kubwa ya wazazi kughalimika kutoka katika nchi mbalimbali ili kuwatembeza katika Jiji la Barcelona na makao makuu ya Barcelona.

    Msimu uliopita, Messi alitengeneza hadi dola milioni 41.3 (zaidi ya Sh bilioni 88), ni bilionea lakini si rahisi kumuona akifanya mbwembwe, hili linazidisha umaarufu wake kwa kuonekana si mpenda makuu.


    Kupitia wadhamini tu mfano wa Gillette, Samsung, Gatorade na sasa Huawei, Messi anaingiza zaidi ya dola milioni 22.5 kupitia matangazo hayo tu. Yaani nje ya mpira na kumfanya kuwa kati ya wanamichezo wanaoingiza fedha nyingi sana katika matangazo.

    Kumbuka, Adidas wanamlipa dola milioni 4 (zaidi ya Sh bilioni 8.5) kwa mwaka na kumfanya kuwa mwanamichezo anayelipwa zaidi na kampuni hiyo kubwa ya michezo ambayo inawadhamini wanamichezo mbalimbali duniani.

    Thamani yake kama klabu yoyote ikitaka kumnunua ni dola milioni 340, Barcelona iliwahi kutangaza. Huenda kusiwe na klabu nyingine yoyote inaweza kumnunua.

    Lakini hata kubaki naye tu, Barcelona haina shida wala shaka kwa kuwa inaendelea kuingiza mamilioni ya fedha ikimtumia yeye kama chanzo cha biashara.

    Messi ni faida kwa klabu yake ya Barcelona, lakini ni faida kubwa kwa wakazi wa Jiji la Barcelona ambao wanafaidika kwa yeye tu kuwa mkazi wa jiji hili.

    MO DEWJI AANZA NA MISHAHARA SIMBA SC




    MFANYABIASHARA anayetaka kununua hisa ndani ya Klabu ya Simba, Mohamed Dewji ‘Mo’, ameanza kasi ya kuitumikia klabu hiyo ya Simba kwa kuanza kulipa mishahara ya wachezaji kuanzia mwezi huu huku suala la kununua hisa likitarajiwa kukamilika ndani ya mwaka mmoja.Hatua hiyo ya Mo imekuja baada ya Kamati ya Utendaji ya Simba kuridhia kubadili mfumo wa uendeshaji wa klabu kutoka wa sasa wa wanachama na kwenda kwenye mfumo wa hisa, kufuatia Mo kuhitaji kununua hisa asilimia 51.
    Aidha, kamati itaandaa mkataba wa maridhiano ili kila upande uweze kutekeleza majukumu yake ambapo Mo alieleza kuwa ataisaidia timu hiyo huku akiwa anaendelea kusubiria mchakato wa hisa kukamilika.
     

    Akizungumza mjumbe mmoja wa Kamati ya Utendaji Simba ambaye aliomba jina lake lifichwe, alisema Mo ataanza kuwalipa wachezaji mishahara kuanzia mwezi huu.
     

    “Kwa sasa kuna kamati imepewa kazi ya kuwaelimisha wanachama juu ya suala hilo ili kuweza kufahamu faida gani watakayoipata juu ya suala hilo ili mwisho wa siku yafanyike maamuzi sahihi.
     

    “Kwa kuanza, ataanza na kuwalipa mishahara wachezaji ambapo itaanzia mwezi huu na atapewa majina ya wachezaji wanaotakiwa kulipwa mishahara ili aweze kuwalipa wachezaji wote lakini jukumu alilopewa ni juu ya timu tu kwa sasa lakini mambo mengine yote yatabaki chini ya uongozi.
     

    “Suala lake nadhani litachukua muda mrefu hata mwaka mmoja hadi kufikia kukamilika kwa mchakato mzima kufuatia kupata maoni mbalimbali na makubaliano kutoka kwa wanachama baada ya kupata elimu ya kutosha.
    “Hata hivyo asilimia kubwa ya wanachama hawataki auziwe hisa kubwa ya asilimia 51 na badala yake auziwe asilimia 48,” alisema bosi huyo.
     

    Alipotafutwa Msemaji wa Simba, Haji Manara kuzungumzia suala hilo, simu yake iliita bila ya kupokelewa hata katibu, Patrick Kahemele naye simu yake haikupokelewa.
    Tayari Mo alishatoa msaada wa shilingi milioni 100 kwa ajili ya kusaidia usajili, kiasi ambacho Simba ilikitumia kwa ajili ya kukamilisha usajili wa wachezaji kadhaa nyota walionao hivi sasa.

    Saturday, August 20, 2016

    ACHANA NA POGBA, UMESIKIA MOURINHO ALICHOSEMA KUHUSU FELLAINI? HIKI HAPA…


    Wakati dunia ikiamini kuwa kiungo Marouane Fellaini atakuwa mmoja wa wachezaji ambao wataondoka klabuni hapo mara baada ya kutua kwa Kocha Jose Mourinho hali imekuwa tofauti kabisa na vile ambavyo ilikuwa ikitegemewa.

    Fellaini ambaye ameanza katika mechi zote za ushindani chini ya kocha huyo alionyesha kiwango kizuri katika mchezo wa timu yake hiyo dhidi ya Southampton, juzi na kuwashangaza wengi waliojua kuwa safari yake imewadia.   






     Akizungumzia juu ya kufanya vizuri kwa mchezaji huyo ndani ya muda mfupi licha ya wengi kumuona ameshindwa maisha ndani ya klabu hiyo maarufu kwa jina la Mashetani Wekundu, Mouringo alifafanua kuwa yawezekana yote hayo yalianza kutokana na simu.

    “Naweza kusema kuwa labda simu ilichangia kwa kuwa mara baada ya kiutambulishwa tu kuwa nimekuwa kocha wa United nilimpigia simu.

    “Nadhani hata yeye hakutegemea kwa kuwa alijihisi ni mchezaji ambaye hapendwi hapa, lakini yawezekana simu ilirejesha kujiamini kwake na ndiyo maana nacheza vizuri sasa,” alisema Mourinho.

    Fellain, kiungo wa zamani wa Everton ambaye alishindwa kuwa na maisha mazuri klabuni hapo kuanzia kwa kocha David Moyes ambaye ndiye aliyemsajili na hata kwa Louis van Gaal ambaye alitimuliwa msimu uliopita.

    ACHANA NA USAIN BOLT, HUYU JAMAA ANAKIMBIA BANA, ABEBA DHAHABU NYINGINE OLIMPIKI.

    ````Mwanariadha wa Jamaica, Usain Bolt amekamilisha ubabe wake wa kuchukua medali tatu ikiwa ni mara ya tatu kufanyua hivyo kwenye michezo ya Olimpiki.






         Bolt amefanya hivyo baada ya kukamilisha kupata medali ya dhahabu katika Olimpiki ambayo inaendelea nchini Brazil kwa kuchukua medali ya dhahabu katika mbio za mita 400 akiwa na wenzake wengine wane, ambapo walikuwa wakipokezana vijiti.
      
    Bolt ambaye kabla ya hapo alikuwa na medali ya dhahabu katika mita 100 na mita 200 aliwaongoza wenzake kushinda kwa kukimbia kwa sekunde 37.27 wakifuatiwa na Wajapani waliokimbia kwa sekunde 37.60 huku Wacanada wakishika nafasi ya tatu kwa sekunde 37.64.

    Waingereza waliokuwa wakijipa matumaini ya kufanya vizuri walishika nafasi ya tano kwa kukimbia sekunde 37.98.